August 6, 2012

SIJATUMWA NA MWANACHAMA YEYOTE KUGOMBEA UENYEKITI UWT IRINGA ASEMA ZAINAB MWAMWINDI

Katibu wa umoja wa wanawake Tanzania (UWT) mkoa wa Iringa Christina Kibiki (kushoto) akipokea fomu kutoka kwa mwenyekiti wa UWT mkoa wa Iringa anayemaliza muda wake Zainab Mwamwindi ambaye ni miongoni mwa wanachama watatu waliojitokeza hadi leo jioni kugombea nafasi hiyo ya kiti mkoa wa Iringa
WAKATI heka heka za uchaguzi wa viongozi ndani ya chama cha mapinduzi (CCM) zikiendelea kupamba moto kwa wanachama wake kujitokeza kuchukua fomu na kurejesha ,mwenyekiti wa umoja wa wanawake Tanzania (UWT) mkoa wa Iringa Zainab Mwamwindi amesema kuwa amejitosa kutetea nafasi hiyo kwa mara ya pili pasipo kushinikizwa na mgombea yeyote wa UWT ngazi ya Taifa na kuwa yeye si mpiga debe wa Shopia Simba wala Anne Kilango Malecela.

Akizungumza na mtandao huu wa www.francisgodwin.blogspot.com leo katika ofisi za UWT mkoa wa Iringa Zainab Mwamwindi alisema kuwa makundi ndani ya CCM ndio ambayo yanachangia kuua chama na kuwa wanachama wanaogombea kwa ajili ya kuwapigia debe wanachama wa kitaifa walioomba nafasi za juu ni kosa na wanapaswa kuacha mara moja tabia ya kugombea kwa ajili ya kutengeneza daraja la mgombea mwingine.

Mwamwindi alisema kuwa ili chama hicho cha CCM kiendelee kusonga mbele ni lazima wanachama wenye mapenzi mema kuendelea kujitokeza kuwania nafasi ndani ya chama bila ya kutengeneza kundi lolote .

Kwani alisema iwapo wanachama wanaingia katika nafasi mbali mbali ndani ya chama huku wakiwa na makundi ni hatari ndani ya chama na kuwa wanachama wa aina hiyo wanapaswa kuogopwa zaidi.

Kuhusu wanachama wa UWT ambao wanatoka ndani ya CCM na kujiunga na upinzani aliwataka wanachama hao kuacha kufanya hivyo kwani alisema kuwa pamoja na kuwa baadhi ya vyama vya upinzani kuendesha kampeni chafu za kukichafua chama ila bado CCM ndicho chama Imara na kuwa kuhama chama si njia sahihi ya kuendelea kuleta mageuzi ya kweli ndani ya chama.

Hata hivyo alisema kuwa akiwa mwenyekiti wa UWT mkoa wa Iringa amepata kuwaunganisha wanawake kuwa kitu kimoja na kuwa iwapo atachaguliwa tena ataendelea kuwa kiunganishi kizuri katika UWT na CCM .

Aidha alisema katika kampeni zake kamwe hatafanya kampeni za kumchafua mgombea uyeyote wala kukichafua chama na badala yake atakuwa mfano mwema kwa wagombea kwa kufanya kampeni za kistarabu na kuwataka wagombea wengine kufanya kampeni za kukijenga chama badala ya kuchafua chama.

Kwa upande wake katibu wa UWT mkoa wa Iringa Christina Kibiki alisema mbli ya Zainab Mwamwindi wengine waliogombea nafasi hiyo ni pamoja na Nicolina Lulandala ambaye ni mwenyekiti wa UWT Iringa mjini na diwani wa kata ya Gangilonga , na Augusta Mtemi .

MWISHO

No comments: